Balozi Mwanaidi atetea
haki za Wafanyakazi wa ndani ughaibuni
22/02/2010

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza,
Mheshimiwa Mwanaidi Maajar, amependekeza kukazwa sheria za kuwalinda
wafanyakazi wa ndani wanaosafirishwa kufanya kazi za utumishi nchi za
kigeni.
Akiongea nami jana Jumapili mjini London,
Mama Maajar alikuwa akitoa maoni kuhusu kukamatwa na kuchunguzwa na
polisi kwa baadhi ya waajiri wa Kitanzania hapa Uingereza wanaowaleta
wafanyakazi wa ndani na kutotimiza ahadi walizowapa kabla ya safari.
“Tunachokiona ni kuvunjwa kwa makubaliano
ya kuaminiana kati ya wafanyakazi na waajiriwa,” alisisitiza.
Mwezi Desemba mwaka jana maofisa wawili wa
polisi wa Kiingereza walisafiri Bongo kwa majuma mawili kama sehemu ya
uchunguzi wa mateso aliyofanyiwa Bi. Zubeda Ali na waajiri wake, mjini
Birmingham toka 2007.
Waajiri hao, Bwana na Bibi Shariff, ambao
wamewekewa dhamana hadi kesi yao itakapofikishwa tena mahakamani mwezi
ujao walitiwa hatiani mwezi jana kwa mashtaka ya kusafirisha wanadamu
kinyume cha matakwa yao na kukiuka masharti ya uhamiaji.
Mwishoni mwa wiki jana mwajiri wa
mfanyakazi mwingine wa makamo mzawa wa Kondoa alihojiwa na polisi wa
London baada ya mfanyakazi huyo kupelekwa hospitali akiwa na ugonjwa wa
kuvimba miguu (Varicose Veins).
Bibiye alifanya kazi kutwa kucha bila
mapumziko wala likizo na kulala jikoni. Mshahara wake mdogo (shilingi
elfu 20) alipewa mwisho wa mwaka si kwa mwezi. Mwajiri wake alimwita kwa
kengele kama mbwa badala ya kutumia jina lake. Kwa sasa anahifadhiwa na
kutetewa na chama kinachopigania maslahi ya wafanyakazi wa ndani (Kalaayan)
na Umoja wa Wanawake wa Tanzania London (TAWA).
Balozi Maajar kasema wafanyakazi hawa wa
ndani hudanganywa kwamba watalipwa vizuri na waajiri wao. “Wakiambiwa
watalipwa shilingi laki mbili ughaibuni wanaona nyingi lakini punde
wanakutana na maisha tofauti na yale waliyoahidiwa.”
Mheshimiwa Maajar alisema Ubalozi wa
Tanzania umekuwa ukishirikiana na taasisi mbalimbali husika hapa, polisi
wa Uingereza na TAWA kuwasaidia wanawake hawa.
Ila alisema tatizo hili halipo UIngereza
tu. “Karibuni nimesoma habari mtandaoni kuhusu unyanyasaji wanaofanyiwa
wafanyakazi wa Kibongo nchi za Uarabuni.”
Aliendelea kueleza kuwa wengi wa waajiri
hawa ni watu wanaoheshimiwa Bongo na hawakubali kwamba wanachokifanya si
kizuri. Wamezoea kuwafanya binadamu wenzao watumwa.
“Iko haja ya kuwafichua maana majina yao
yameshawekwa hadharani hapa na kesi ziko mahakamani. Je, watajisikiaje
kama hawa wanawake wangekuwa binti zao?”.
Habari na Freddy Masha.
|