Benki ya Exim China yaipa
Tanzania msaada wa milioni 170 za Marekani
15/04/2010

Waziri wa fedha na uchumi Mustafa mkulo
kulia akibadilishana hati na makamu wa rais wa benki ya Exim ya China
Zhu Hongjie ikiwa ni makubaliano ya mkopo wa dola milioni 170 za
marekani kwa ajili ya uendelezaji wa mkongo wa mawasiliano wa taifa na
uendelezaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar.
Benki ya Exim ya China imetiliana saini na
Serikali ya Tanzania makubaliano ya mkopo kwa ajili kusaidia miradi
miwili ya maendeleo nchini Tanzania. Makubaliano hayo yalifikiwa jijini
Dar es salam kati ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na Makamu
wa Rais wa Benki ya Exim, Zhu Hongjie. Katika mradi wa kwanza Benki hiyo
imetoa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa
Mkonga wa Taifa wa mawasiliano awamu ya pili (broadband).
Kwa mujibu wa Waziri wa fedha na Uchumi,
Mustafa Mkulo, mkopo huo utasaidia kuimarisha mawasiliano ya Teknolojia
(ICT) ikiwemo uboreshaji wa huduma za tovuti na simu. Alisema kuwa
msaada huo utasaidia kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali kupitia
teknolojia ya mawasilano (ICT) na hivyo kuondoa umaskini. Aidha, Mkulo
alisema kuwa pia EXIM Benki ya China itatoa Dola milioni 70 kwa ajili ya
kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Alisema kuwa hatua hiyo itarahisisha
usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo. Mkulo alisema mara baada ya
kukamilika kwa uboreshaji wa uwanja huo wakazi na wananchi wa Zanzibar
hawana haja ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za usafiri
badala yake watatumia uwanja huo. Katika hatua nyingine, Waziri Mkulo
ametoa wito kwa wananchi wa China kuja kuhudhuria Mkutano wa Dunia wa
Biashara utakaofanyika mapema nchini ili kuja kutafuta fursa za
uwekezaji. Alisema mkutano huo unatarajia kujumuisha zaidi ya watu
maarufu 800 kutoka sehemu mbalimbali duniani.
|