Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Hati ya Nyumba

10/05/2010

Katika historia tunajifunza kwamba katika jamii mbalimbali ardhi ndiyo ilikuwa njia kuu ya uchumi, lakini pamoja na sifa zote hizo ilizonazo, ardhi inaweza kukunufaisha kama utajua kuitumia kwa kadri sheria inavyoruhusu.

Kimsingi kwa mujibu wa sheria, ardhi inamilikiwa na serikali na wananchi wake hupewa umiliki wa muda tu kwa mujibu wa sheria kuanzia miaka 33 hadi 99 kutegemea na maombi na matumizi yaliyokusudiwa na mwombaji.

Ili kupata uhalali wa umiliki wa ardhi, mwombaji anaweza kutambulika kama mmiliki kwa kutumia sheria ya kimila ambayo inatambua umiliki wa ardhi kwa Mtanzania ambaye itadhihirika kuwa bila ya shaka alikuwa akiimiliki tangu kipindi cha kale na mamlaka za eneo husika zinatambua umiliki wake huo.

Inawezekana kabisa hati ya ardhi yako ikapotea na usijue pa kuipata tena kama zinavyoweza kupotea nyaraka nyingine katika mazingira ambayo tumezoea kuyatambua kama ni bahati mbaya.

Lakini pia ni kutokana na unyeti wake katika maisha ya wanadamu, ni rahisi ardhi kufanyiwa hujuma na mtu yeyote na mara nyingi na mtu au watu unaowaamini na wakaribu katika maisha yako ya kila siku kuhusika na upotevo wa kiwanja chako.

Awe rafiki yako kipenzi, mwanao au hata wakati mwingine mkeo au rafiki yako wa kike au kiume kuamua kuificha hati ya nyumba au kuwanja chako akiamini mwisho wa siku anaweza kuuza nyuma ya mgongo wake na kujipatia fedha kwa njia rahisi kwa sababu tu anatumia hati halisi katika kufanya biashara hiyo.

Hii inatawaliwa na dhana potofu miongoni mwa wananchi kwamba ukiwa na hati halisi hata ya kiwanja ambacho si chako kimsingi ndiyo una nguvu na mamlaka ya kufanya utakacho juu ya kiwanja au nyumba husika.

Kwa msimamo wa taratibu za kisheria kuiba au kuficha hati ya mtu mwingine haina maana au athari yoyote katika umiliki wake juu ya ardhi husika zaidi ya kusumbuana na kupotezeana muda tu na wakati mwingine hata kukusababishia kuishia jela kwa tuhuma za wizi au utapeli.

Ni vyema pindi baada ya kutambua kwamba hati yako ya nyumba au kiwanja haionekani na huna taarifa sahihi za kupatikana kwake kuanza kwa kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu nawe na baada ya hapo utapatiwa hati maalumu ya taarifa ya kupotelewa ambayo ndiyo itatumika kama leseni ya kutambulika kwa maelezo yako katika ofisi za ardhi husika.

Baada ya kukamilika kwa taratibu zote hizo za msingi ikiwa ni pamoja na kuijaza fomu maalumu za kisheria ambazo huandaliwa na wanasheria mbalimbali ofisi ya ardhi husika hubatilisha hati iliyopotea na kukupatia kivuli cha hati halisi ambacho kufuatia kufikishwa na kukubalika kwa taarifa hizo katika ofisi husika ya ardhi hati halisi iliyotolewa ndiyo huchukua nafasi ya hati halisi.

Kwa maana hiyo ndiyo kusema kwamba pindi baada ya kuidhinishwa kwa uhalali wa kutumia hati kivuli, hati halisi popote ilipo huwa si halali tena na yeyote ambaye ataitumia kwa namna yoyote ile iwe kuuza au kuchukulia mkopo katika benki au taasisi yoyote ya fedha atakuwa anakinzana na sheria ambayo haitasita kuchukua mkondo wake dhidi yake.

Mchakato wa kutoa taarifa na kushughulikia kupatikana kwa hati mpya unalazimika kufanyika mapema iwezekanavyo pindi baada ya kutambua upotevu wa hati husika ili kuepuka kutoa nafasi kwa aliyeichukua kwa nia mbaya kuweza kufanya taratibu za uhamisho kabla ya mhusika.

Hii ni kuhimiza umuhimu wa kuangalia na kupitia mara kwa mara hifadhi ya nyaraka majumbani kwetu ili kuepuka kuja kushtuka wakati mwizi wako ameshafanya taratibu zote muhimu zinazokubalika na zisizokubalika ilimradi tu kukupoka haki yako ya umiliki wa ardhi.

Utaratibu huu utarahisisha kujiridhisha kwako juu ya usalama wa nyaraka zako muhimu na hata kuweza kuchukua hatua za haraka baada ya kugundua upotevu wa hati husika.

Utaratibu wote huu mpaka kupatikana kwa hati vivuli huchukua muda mfupi na kuhusisha gharama ndogo isiyozidi 10,000 za Kitanzania bila ya kujali thamani ya ardhi au nyumba husika.

Hivyo ni vyema kwa yeyote mwenye kupotelewa na hati kukimbia katika ofisi za ardhi mapema baada ya kujiridhisha kuwa hati husika haipo mahala pake kama alivyokuwa amehifadhi awali badala ya kuhangaika kutafuta mpaka mahala kusikotafutika.

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©