Mzee Pwagu afariki dunia
28/05/2010

Aliyekuwa mwigizaji mahiri redioni Rajab Kibwana Hatia al maaruf
Mzee Pwagu amefariki dunia. Mzee Pwagu amefariki leo Ijumaa, Mei
28, 2010 katika hospitali ya Amana jijini Dar Es Salaam kutokana na
kusumbuliwa na kwikwi na hali ya uzee.
Mzee
Pwagu alikuwa anakamilisha pacha wake Mzee Pwaguzi katika kipindi cha
redio kilichokuwa maafuru sana miaka ya sitini hadi themanini
kilichojulikana kwa jina la Pwagu na Pwaguzi.
Kipindi hicho kilikuwa kikirushwa hewani kila siku ya Jumamosi saa kumi
na moja na dakika arobaini na tano jioni hadi saa kumi na mbili kamili
(11:45 - 12:00) kupitia Redio Tanzania Dar Es Salaam (RTD). Kwa mara ya
kwanza kipindi hicho kilianza kusikika mwaka 1966 na kilipendwa
kusikilizwa na watu wa rika zote kutokana na kuelimisha na kutoa
burudani inayogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania, hadi mwaka 1980
kilipokoma.
Marehemu alikuwa akiishi Kigogo Mbuyuni jijini Dar Es Salaam na
anatarajiwa kuzikwa kesho. Apumzike pema Rajab Kibwana Hatia/Mzee Pwagu.
Historia fupi ya Mzee Pwagu
Pwagu alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora na kuanza elimu yake katika
shule ya msingi Tabora Town mwaka 1942.
Kabla hajamaliza elimu hiyo ya msingi, Pwagu alihamishiwa jijini Dar es
Salaam alikojiunga na shule moja ya seminari iliyokuwa ikifahamika kwa
jina UMCA, Minaki. Hata hivyo msanii huyo ambaye anasema uwezo wake
katika maigizo aliuanzia akiwa hapo, hakuwahi kumaliza masomo yake hayo
baada ya kutakiwa aende Mombasa kujiunga na kozi nyingine.
“Desemba 1942 alikuja Mzungu mmoja aliyeitwa Donald Brown Skout pale
shuleni kwetu na kuuliza iwapo yupo anayetaka kumsaidia King George.
“Mimi na wenzangu tukawa sehemu ya waliokubali kazi hiyo ya kumsaidia
Mfalme huyo aliyekuwa akipigwa na watu mbalimbali akiwemo Adolf Hittler,”
anasimulia.
Walipopelekwa Mombasa, Kenya kwenda kujifunza, mafunzo ambayo
yaliwachukuwa mwaka mmoja tu na baadaye wakapangiwa kazi. “Mimi nilianza
kuingia kwenye meli ya kivita iitwayo H.A. Losaland ambayo ilikuwa
ikizunguka takriban bahari yote ya Hindi hadi mwaka 1946,”anazidi kuweka
wazi Pwagu.
Mwaka
huo wa 1946 alirejea Dar es Salaam na kufanya kazi Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa kama fundi mchundo, kazi ambayo kwa mujibu wa msanii huyo
alitakiwa aiache na wazazi wake kwa maelezo kuwa ilikuwa ni hatarishi
kwake.
Mwaka
1948 alipelekwa kwenye meli iliyokuwa ikiitwa ACT na kuwa baharia hadi
mwaka 1949.
Mmoja
kati ya watoto wake ndiye mama mzazi wa msanii chipukizi Abdul Ahmad
Salum maarufu kwa jina la Mr Benny wa Kaole.
Makala kumhusu Mzee Pwagu
(Novemba
13, 2009)
NI matumaini yangu kwamba Watanzania wengi watakuwa wanalikumbuka vema
jina la Mzee Pwagu. Na watakaoenda mbali zaidi hawatolisahau pia jina
pacha na hilo la Pwaguzi.
Walio
wengi huthubutu kudhani hivyo kutokana na ukweli kwamba, licha ya kuwa
ni miongoni mwa wasanii mahiri wa michezo redioni, lakini pia alikuwa
hodari katika kipindi maarufu kilichofahamika kwa jina la Wakati wa
Pwagu na Pwaguzi.
Kipindi hicho kilichokuwa kikirushwa hewani kila Jumamosi kuanzia saa
11:45 hadi 12;00 jioni na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) tangu mwaka
1966, kiliweza kukusanya rika zote za wasikilizaji.
Kwa
mujibu wa Pwagu, kipindi hicho kiliendelea mpaka mwishoni mwa miaka ya
1980 kilipopotea kabisa, enzi ambazo kulikuwa hakuna utitiri wa vituo
vya redio.
Akizungumza nyumbani kwake Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam wiki hii,
Pwagu ambaye jina lake halisi ni Rajab Kibwana Hatia, anasema lengo
kubwa la igizo hilo ilikuwa ni kuonesha umuhimu wa uaminifu katika jamii.
Anasema: “Lengo letu kubwa lilikuwa ni kuionesha jamii kuwa hii ngozi
nyeusi ina matatizo katika suala zima la kuaminiana, watu wawili, watatu
au zaidi wanaweza kukubaliana jambo katika biashara, lakini ikatokea
baadhi yao wakawa si waaminifu”.
Mbali
na hilo, anasema kuwa, michezo hiyo pia ilikuwa inalenga kuelimisha
jamii juu ya uwepo wa baadhi ya watu wenye mawazo mazuri katika
kujitafutia maisha, lakini kwa ukosefu wa elimu ya kutosha pamoja na
miundombinu dhaifu, hufanya wakashindwa kufikia malengo.
Mathalani katika michezo ambayo Pwagu anaielezea na inathibitisha hayo
ni kuwa walianzisha mradi wa zahanati ya kung’oa meno huku wakiwa hawana
mafunzo yoyote ya kazi hiyo ingawa nje ya ofisi yao kulikuwa na bango
kubwa likionesha wataalamu wa kung’oa meno wapo hapo.
“Mteja
alipofika na mgonjwa wake alipokewa mapokezi na mwenzangu Pwaguzi, baada
ya kulipia pesa ya matibabu huja chumbani niliko mimi na kuanza kumng’oa
kwa kutumia koleo za mafundi baiskeli,” anasema kwa lafudhi yake ya
kisanii.
Ukiachana na mchezo huo, vilevile kwa kushirikiana na mwenzake Ali Said
Keto (Pwaguzi) ambaye kwa sasa ni marehemu, walianzisha miradi ya
ushonaji, ujenzi wa madaraja (makandarasi), wauzaji nyama, japo walikuwa
hawana ofisi mahususi, wakipanga chini hali iliyosababisha wakamatwe kwa
kuhatarisha afya za walaji, mafundi rangi na kadhalika.
“Lakini hakuna hata mmoja katika miradi hiyo tuliofanikiwa kuingiza pesa
na tukamaliza kwa usalama bila kushtukiwa na wateja.
"Kana
kwamba haitoshi mwenzangu aliyekuwa akipokea fedha ninapokutana naye
baadaye kuulizia kile kiasi ambacho mteja alitoa, anasema zilishapotea
katika purukushani za kukimbia, jambo ambalo lilizidi kuonesha watu
weusi tusivyo waaminifu,” anabainisha.
Mwandishi alipotaka kujua kama michezo hiyo ilikuwa ni ubunifu wao ama
kulikuwa na mtu nyuma ya pazia aliyekuwa akiwatungia vituko hivyo,
msanii huyo mwenye umri wa miaka 86 anasema; “Ki ukweli ni kwamba hakuna
mtu aliyekuwa akitutungia michezo, bali ni sisi wenyewe.”
Msanii
huyo aliyekuwa akifanya kazi Mamlaka ya Bandari kitengo cha foko kama
dereva, aliweza kushirikiana kwa karibu na mwenzake Pwaguzi ambaye
alikuwa Ofisa Kamisaa wa Michezo Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuandaa
michezo kulingana na jamii ya wakati huo.
Mbali
na wasanii hao nyota, wengine walikuwemo kwenye kundi hilo lililokuwa
likijulikana kwa jina la Raha Leo Radio Tanzania ni pamoja na kiongozi
wake Hamis Tajiri (Janja au Meneja Mikupuo) ambaye ni marehemu.
Wengine ambao kwa mujibu wa Pwagu ni Tunu Mrisho (Mama Haambiliki),
Mwanaheri Ng’andu, Justin Kilumbi, Ali Manjunju (Ngosha), Batholomeo
Milulu (Masawe) na Ibrahim Raha (Mzee Jongo wakati ambapo Fundi Said
Kipara, baadhi wapo hai na wengine wamefariki dunia.
Pwagu
aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa kundi la Sanaa la Kaole lenye makao yake
Dar es Salaam, amesema anasononeshwa sana na hatua ya baadhi ya wasanii
kukiuka maadili ya utamaduni wetu wakati wakifanya shughuli zao.
“Haiwezekani msanii wa kiume awe jukwaani akionekana kama vile mtoto wa
kike, kwa vyovyote vile hii haikubaliki katika jamii inayothamini utu na
maadili,” alieleza.
Bila
kutaja majina ya wasanii wenye mwenendo huo, Pwagu alitumia muda mrefu
kulaani kitendo hicho ambacho alidai kwa sasa kinaonekana kama jambo la
kawaida na ni cha kistaarabu kwa wasanii huku akisisitiza kuwa
kinapingana hata na mafundisho ya dini.
“Kwanza kimavazi wanaacha kabisa maadili ya Kitanzania, wanapenda sana
kuiga mavazi ya kimagharibi na haya sio mavazi mazuri,” anasema.
Akitoa
nasaha zake kwa wasanii chipukizi, Pwagu amewataka warudi nyuma
kuangalia wapi walikotoka na walifanya nini kipindi hicho, na hivi sasa
wako wapi.
Akienda mbele zaidi, Pwagu anakusudia kulifikisha kwenye Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA ), suala la ukiukwaji maadili kunakofanywa na baadhi ya
wasanii, ambao amedai wapo mpaka wanaume wanaosuka nywele pamoja na
kuvaa shanga na vidani.
“Hawa
wakuu wa BASATA wawe wanatembelea kila kikundi kuondoa kitendo hicho kwa
kuwa haivumiliki watu wachache waachwe wakiuchafua utamaduni wetu na wao
wakitazama tu,” anasema huku uso wake ukiwa umebadilika.
Anamuomba Ofisa anayeshughulikia vikundi vya sanaa BASATA kuongeza
juhudi katika kushughulikia suala hilo.
Ingawa
msanii huyo hivi sasa ni mgonjwa kama, ambapo mwandishi wa makala haya
alimkuta amelala chumbani kwake, amesema bado anaendelea kushiriki
kwenye michezo anapohitajika kutengeneza filamu.
“Hivi
karibuni nimecheza mchezo unaoitwa Bint Kimanzi na kundi la Dhahabu
Halisi la Keko kama baba yake Anthony,” anaeleza.
Katika
hatua nyingine, msanii huyo aliutolea uvivu uongozi wa iliyokuwa RTD
ambayo sasa ni TBC Taifa, kwa kile alichodai kuwatupa wasanii hao
wakongwe licha ya kuwa mchango wao mkubwa ulikiwezesha kituo hicho cha
redio kuwa juu.
Anasema awali walipewa ofa ya kutangaziwa vifo vinapotokea kwa watu wa
karibu yao, lakini hivi sasa kitu cha namna hiyo kimeondolewa kabisa
kwao.
“Sisi
tuliambiwa kuwa, tutapewa ofa ya kutangaziwa bure matangazo ya vifo, na
kweli utaratibu huo ulikuwepo huko nyuma. Cha ajabu hivi sasa haupo,”
anasema. Pwagu ambaye sasa ni mshauri mkuu wa Kaole, alizaliwa mwaka
1923 mjini Tabora na kuanza elimu yake katika shule ya msingi Tabora
Town mwaka 1942.
Kabla
hajamaliza elimu hiyo ya msingi, Pwagu alihamishiwa jijini Dar es Salaam
alikojiunga na shule moja ya seminari iliyokuwa ikifahamika kwa jina
UMCA, Minaki.
Hata
hivyo msanii huyo ambaye anasema uwezo wake katika maigizo aliuanzia
akiwa hapo, hakuwahi kumaliza masomo yake hayo baada ya kutakiwa aende
Mombasa kujiunga na kozi nyingine.
“Desemba 1942 alikuja Mzungu mmoja aliyeitwa Donald Brown Skout pale
shuleni kwetu na kuuliza iwapo yupo anayetaka kumsaidia King George.
“Mimi
na wenzangu tukawa sehemu ya waliokubali kazi hiyo ya kumsaidia Mfalme
huyo aliyekuwa akipigwa na watu mbalimbali akiwemo Adolf Hittler,”
anasimulia.
Anasema ndipo walipopelekwa Mombasa, Kenya kwenda kujifunza, mafunzo
ambayo yaliwachukuwa mwaka mmoja tu na baadaye wakapangiwa kazi.
“Mimi
nilianza kuingia kwenye meli ya kivita iitwayo H.A. Losaland ambayo
ilikuwa ikizunguka takriban bahari yote ya Hindi hadi mwaka
1946,”anazidi kuweka wazi Pwagu.
Mwaka
huo wa 1946 anasema alirejea Dar es Salaam na kufanya kazi Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa kama fundi mchundo, kazi ambayo kwa mujibu wa msanii
huyo alitakiwa aiache na wazazi wake kwa maelezo kuwa ilikuwa ni
hatarishi kwake.
Msanii
huyo ambaye hata hivyo aliingia tena majini mwaka 1948, ambapo
alipelekwa kwenye meli iliyokuwa ikiitwa ACT na kuwa baharia hadi mwaka
1949.
Ana
mke na watoto wawili. Mmoja kati ya watoto wake ndiye mama mzazi wa
msanii chipukizi Abdul Ahmad Salum maarufu kwa jina la Mr Benny wa Kaole.
|