Tanzania kupambana na
Brazil katika mechi ya kirafiki 2010
31/05/2010

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) jana
lilitangaza kiingilio cha mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya
soka ya Tanzania, Taifa Stars, na Brazil itakayopigwa Juni 7 huku
kiwango cha juu kikiwa sh 200,000.
Mechi hiyo itakayopigwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, kiwango cha chini kabisa ni shilingi 30,000.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick
Mwakalebela, hadi kufikia jana, tiketi hizo za sh 200, 000 ambazo ni za
jukwaa VIP A, zimekwisha.
Alisema, kulingana na idadi ya viti vya jukwaa hilo, tayari kiasi cha
shilingi mil. 140 zimepatikana na kutaka wananchi wajitokeze kununua
tiketi za maeneo mengine.
Mwakalebela alitaja viwango vya maeneo
mengine ambapo VIP B ni sh 150,000; VIP C sh 100,000; Viti vya rangi ya
chungwa mkabala na VIP, itakuwa sh 80,000 huku viti vya rangi ya chungwa,
nyuma ya magoli itakuwa sh 50,000.
Alisema viwango hivyo vimetokana na gharama kubwa za kuileta timu hiyo,
hivyo kuifanya mechi hiyo kuwa ya gharama kubwa tofauti na mechi
nyingine zilizowahi kuchezwa nchini.
Katika hatua nyingine, mchezaji Ricardo
Kaka hatacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Zimbabwe na ile
itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam baada ya jana
kuumizwa na
Felipe Mello katika mazoezi.
Habari zinasema, Kaka amepata maumivu makali yaliyomfanya kuibuke mzozo
mkali kati yake na Mello na kumfanya Kaka kususa na kuondoka mazoezini.

Matangazo ya mechi ya Tanzania na Brazil
katika magazeti la METRO, UK.
|