Wanawake 21 wajitokeza
kuwania uongozi Zanzibar
01/06/2010

Wanawake 21
wa Zanzibar wametangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama
mbali mbali vya siasa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Oktoba
mwaka huu.
Wanawake hao ni wale ambao wamenufaika na mradi wa kuwawezesha wanawake
kijamii na kiuchumi, Zanzibar (WEZA) unaoendeshwa katika Mkoa wa Kusini
Unguja na Kaskazini Pemba tokea 2008.
Wanawake 13
kati ya hao wanatoka Mkoa wa Kaskazini Pemba na wanane ni kutoka Mkoa wa
Kusini Unguja.
Waratibu wa Shehia za mikoa hizo wamesema wamefurahishwa na uamuzi wa
wanawake hao kutaka kugombea uongozi na kwamba hayo ni maendeleo makubwa
ikizingatiwa kuwa katika chaguzi zilizopita wanawake walikuwa
hawajitokezi kwa wingi kugombea.
Mratibu wa
Shehia ya Tumbe Magharibi, Salma Tumu, ambaye Shehia yake imetoa
wanawake watano wanaogombea, amesema jitihada za kuwawezesha wanawake wa
Zanzibar kujiamini kijamii na kiuchumi zikiendelezwa lengo la kupata
asilimia 50 ya wanawake katika uongozi wa kuchaguliwa litafikiwa
kirahisi.
Raya Majid Salim ambaye ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo
la Tumbe huko Pemba amesema ameamua kugombea kwa sababu anajiamini kuwa
anao uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua
matatizo ya kijamii yanayowakabili wanawake.
“Wanawake sasa tunafahamu haki zetu katika uongozi na kilichobaki ni
kuzipigania ili kuzipata na kuzitumia kwa ajili ya kuharakisha
maendeleleo ya jamii nzima-wanawake, wanaume na watoto”, alisema Raya
Majid Salim.
Aliyataja
matatizo yanayokwamisha maendeleo ya familia na taifa huko Zanzibar
ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na viongozi kuwa ni pamoja na watoto wa
kike kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo na wanaume na wanawake wasio
na kipato kukosa mitaji kwa ajili ya kuendesha miraji ya kiuchumi.
Khadija Omar Kibano ambaye anagombe udiwani wadi ya Mtambwe kaskazini
amewataka wanawake nchini kote kugombea nafasi mbali mbali katika
uchaguzi wa mwaka huu kama wanavyojitokeza wanaume
Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania, Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Umoja wa Ulaya (EU),
Serikali ya Austria na Care Austria.
|