Wakazi wa Jangwani/Kigogo
kufidiwa
03/06/2010

Serikali inatarajia kutumia sh. bilioni 15
kuwalipa fidia wananchi watakaoathiriwa na ujenzi wa barabara ya
Jangwani-Kigogo hadi Ubungo
Maziwa.
Barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha
lami, ikiwa ni mkakati wa kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam
na kuwaondolea usumbufu wananchi wa maeneo hayo.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam,
James Nyabakari, alisema hayo
juzi, alipotoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Waziri wa
Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa.
Nyabakari alisema fedha hizo zitatumika kuwalipa fidia wenye nyumba
zilizo kando mwa barabara hizo na kuhamisha miundombinu ya maji, umeme
na simu. Alisema barabara inayoanzia mtaa wa
Twiga hadi Kigogo Mbuyuni,
ambayo ujenzi wake utatekelezwa katika awamu ya pili, wananchi
watafidiwa sh. bilioni nne.
Meneja huyo alisema barabara ya kutoka
Kigogo Mbuyuni hadi Ubungo Maziwa,
ambayo ujenzi wake upo katika awamu ya kwanza, sh. bilioni 12 zitatumika
kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi. Dk. Kawambwa alisema ujenzi wa
barabara hiyo ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuboresha
miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam. Aliagiza uhakiki ufanyike kwa
umakini, ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza wakati wa ulipaji
fidia. "Ninawaomba mfanye uhakiki wa kina kusije kukajitokeza migogoro
baadae, natarajia katika kikao cha Bunge kitakachoanza hivi karibuni
nitaomba ridhaa ya kutumia fedha hizo," alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, iwapo makadirio ya matumizi ya fedha ya
wizara yatapitishwa na Bunge, miradi hiyo itaendelea kutekelezwa. Alisema
watakaoathiriwa na mradi huo watatafutiwa eneo mbadala kwa ajili ya
makazi na kwamba, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa
barabara hiyo.
|