Kwa mujibu wa waandaaji wa mechi hiyo, Mamlaka ya Utalii ya nchini
Zimbabwe -- Zimbabwe Tourism Authority (ZTA)-- baadhi ya fedha bado
zinaendelaa kukusanywa kutoka katika makampuni ambayo yalinunua
tiketi hizo kwa ajili ya wafanyakazi wao walioketi katika viti vya
watu maarufu na wale maafuru sana (VVIP and VIP).
Waandaaji hao wanasema kuwa walitoa tiketi za bure (complimentary
tickets) kwa mabalozi mbalimbali na makampuni kadhaa ila cha
kushangaza ni kuwa, tiketi hizo za bure ziliuzwa kinyemela na watu
kuingia nazo kiwanjani na hivyo kuwasababishia waandaaji hao kukosa
mapato ya tiketi hizo. Kituo cha radio cha VOP kinaripoti kuwa
kilifanikiwa kuiona tiketi ya VVIP ikiuzwa kinyemela nje ya Uwanja.
Vijana wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Samba Boys, walilipwa kitita
cha jumla ya dola milioni 2.5 kwa ajili ya kucheza mchezo huo.
Serikali imefikia asilimia 45% ya gharama ilizotumia katika mechi
hiyo wakati kwa upande wa makampuni, wengi wao hali haikuwa kama
walivyotarajia kwani timu ya taifa ya Brazili ilichukua nafazi zote
za matangazo katika mechi hiyo. Wachuuzi wadogo wadogo nao
wamefurahia ujio wa Brazili kwani waliripoti ongezeko la kipato
kutoka kwenye biashara zao walizozianza tangu asubuhi katika maeneo
ya kiwanja hicho.
Mchezaji mashuhuri wa Brazili, Kaka aliwafurahisha watazamaji
waliofika kiwanjani mara baada ya kipenga cha mwisho kulia, kwa
kuwarushia jezi yake "sandakalawe" kwa ajili ya kumbukumbu kwa
atakayeipata, nao wachezaji wa Zimbabwe walifanya hivyo.
Timu ya Brazili itashuka katika kiwanja cha mpira wa miguu cha Taifa
ili kucheza na timu ya Tanzania, Taifa Stars. Tiketi kwa ajili ya
mechi hiyo zimekuwa zikiuzwa na TFF kwa kati ya dola 25 hadi 180
kutegemea na watakakoketi watazamaji. Inasemekana kuwa TFF wamelipa
kiasi cha dola za Kimarekani milioni 2.5 kwa Brazili kwa ajili ya
kuipata mechi hiyo.