Bajeti SMZ hakuna kodi
mpya
11/06/2010

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
imewasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2010/11 bila kupandisha
kodi kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wake.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi katika kikao cha Baraza la
Wawakilishi jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk.
Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema serikali imechukua hatua hizo ili
kupunguza mfumuko wa bei katika soko la ndani.
Dk. Mwadini alisema bajeti ya mwaka huu imeathiriwa na nakisi kwa Sh.
milioni 6,000, lakini alisema pengo hilo litazibwa na mikopo ya ndani
kupitia hati fungate.
Alisema kuwa serikali inatarajia kutumia Sh. bilioni 444.637 katika
mwaka wa fedha 2010/11 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji
mpango wa maendeleo.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 193.433 zitatumika kwa kazi za
kawaida wakati Sh. bilioni 251.204 zitatumika kwa utekelezaji wa mpango
wa maendeleo na Sh. bilioni 82.459 kwa malipo ya mishahara ya watumishi
wake.
Waziri Mwadini alisema pato la taifa limeongezeka hadi kufikia Sh.
milioni 878.403 kutoka Sh. milioni 748.057 mwaka 2008 sawa na ongezeko
la asilimia 17.4.
Alilieleza Baraza la Wawakilishi kwamba uchumi wa Zanzibar umekuwa
umeongezeka kwa asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.3 kutokana na mageuzi
katika sekta ya kilimo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii.
Alisema pato la mtu wa kawaida pia limeongezeka kutoka Dola za Marekani
milioni 557 hadi 728.364 mwaka 2008 sawa na ongezeko la asilimia 4.3 na
kuwataka wananchi kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu wakati
huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, alisema mfumuko wa bei katika soko la ndani la Zanzibar
umeongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2000 hadi asilimia 9.7 mwaka huu,
lakini alisema mwaka 2008 mfumuko wa bei ulikuwa mkubwa baada ya kufikia
asilimia 20.6 na kuathiri wananchi wake.
Waziri Mwadini alisema kwamba tayari Serikali imeshaanza kupitia upya
muundo wa watumishi wa umma ili iweze kuboresha maslahi yao kwa lengo la
kuwapunguzia ukali wa maisha.
“Maslahi ya wafanyakazi yatashughulikiwa vizuri zaidi baada ya
kukamilika mapitio ya muundo wa watumishi wa umma,” alisema Waziri huyo.
Watumishi wa umma wamekuwa wakilipwa mshahara wa Sh.100,000 viwango
ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wafanyakazi pamoja na vyama vya
wafanyakazi Zanzibar.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inatarajia kukusanya Sh.
milioni 171,687 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani sawa na asilimia 17.9
ya pato la taifa.
Hata hivyo, alisema kwamba katika bajeti hiyo Sh. bilioni 266.950
zinatarajiwa kutoka kwa wafadhili kupitia misaada ya kibajeti kwa ajili
ya utekelezaji programu na miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha
ujao.
Waziri Mwadini alisema kutokana na wahisani kupunguza misaada ya
kibajeti katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya Zanzibar itaathiriwa na
upungufu wa Sh. bilioni 18, lakini serikali imeshaanza kuchukua hatua
mbali mbali kuziba pengo hilo kupitia mikopo.
Aidha alisema kwamba serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya
Jimbo ili kuharakisha maendeleo katika majimbo 50 ya Zanzibar.
Alisema kwamba serikali inatarajia kuwasilisha muswaada wa sheria wa
kuanzisha mfuko huo mwaka huu kama ilivyo kwa serikali ya Muungano
ambayo imeshaanza kutoa fedha za maendeleo ya jimbo kwa wabunge wa
Tanzania Bara na Zanzibar.
|