Mount Kilimanjaro

Beit El Ajaib
     

HomeNewsServicesEventsAbout UsContact Us

 
ProfileToolsGamesCommunity

NEWS

 
 

Ikulu yavunja ukimya juu ya gari la Rais Kilimanjaro

03/06/2010

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KAMA ambavyo mmekuwa mnaandika na kutangaza ni kwamba Jumanne, Juni 8, mwaka huu, 2010, magari yanayombeba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyokuwa yametangulia kumsubiri Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa ajili ya ziara yake ya siku mbili mkoani Kilimanjaro yalishindwa kuwaka baada ya kuwa yamewekewa mafuta kwenye Kituo cha Rafiki kilichoko kwenye Mzunguko wa Barabara wa Arusha Road mjini Moshi.

Suala hili limezua mjadala mkubwa, na linaelekea kupotoshwa kwa kiasi fulani na baadhi ya vyombo vya habari. Ili kuuwezesha umma wa Watanzania kufahamu ukweli na undani wa kilichotokea siku hiyo tunapenda kutoa ufafanuzi wa tukio hilo kama ifuatavyo:

  1. Kwamba asubuhi ya siku hiyo ya Jumanne, wiki hii, kiasi cha saa tano asubuhi, magari matano, aina ya Toyota Land Cruiser, ambayo ni sehemu ya magari yanayombeba Mheshimiwa Rais, baada ya kuwa yamepitishwa katika taratibu zote za maandalizi, yalifika kwenye Kituo cha Rafiki kunywa mafuta ikiwa ni maandalizi ya mwisho kabla hayajaenda kumpokea Mheshimiwa Rais kwenye Uwanja wa Ndege wa KIA. Baada ya kujazwa mafuta, magari matatu kati ya hayo yalikataa kuwaka, na kuona hivyo uamuzi ukachukuliwa kutokuyawasha kabisa yale mengine mawili.

  2. Kwamba Kituo hicho cha mafuta ni moja ya vituo ambavyo vimekuwa vinatumiwa kujaza mafuta ya magari ya Mheshimiwa Rais siku nyingi, na wala magari ya Mheshimiwa Rais hayakwenda kujaza mafuta kwenye kituo hicho kwa kushtukiza ama kwa bahati tu kwa sababu uamuzi wa wapi magari ya Mheshimiwa Rais yanakunywa mafuta haufanywi na madereva wa magari hayo.

  3. Kwamba mpaka yanaingia kwenye Kituo hicho, magari hayo yalikuwa mazima, imara na salama kwa ajili ya kwenda kumpokea Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa anatokea Dar es Salaam, na kuwa tatizo lilianza baada ya kuwa yamejazwa mafuta.

  4. Kwamba pamoja na tatizo hilo, bado msafara wa Mheshimiwa Rais ulipokelewa kama ilivyokuwa imeandaliwa bila tatizo lolote, kwa sababu misafara ya Mheshimiwa Rais inakuwa na mipango mbadala ya usafiri yenye kiwango kile kile cha juu kabisa cha usalama.

  5. Kwamba magari yaliyopata tatizo la mafuta hayakutumika katika msafara huo wa ziara ya Mheshimiwa Rais katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu yalikuwa bado yanasafishwa. Baada ya kuwa yamesafishwa na kuwekewa mafuta mengine yameweza kuwaka, na sasa yako njiani kurejea Dar es Salaam.

  6. Kwamba uchunguzi wa tukio zima sasa uko mikononi mwa vyombo husika vikiwamo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA). Uchunguzi huo ukikamilika wananchi watajulishwa nini hasa kilisababisha magari hayo kuzima baada ya kuwekewa mafuta.

Huo ndio ukweli wa tukio lile la Jumanne mjini Moshi, na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inapenda kuwahakikishia wananchi yafuatayo:

  • Kwamba tukio hilo hakuliathiri kwa namna yoyote ile ama hata kugusa usalama wa Mheshimiwa Rais ama mipango yake ya ziara yake Mkoani Kilimanjaro. Ziara ilikwenda na kufanyika kama ilivyopangwa, tena kwa mafanikio makubwa sana.

  • Kwamba tukio hilo halikusababishwa na uzembe ama kutojali kwa maofisa waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za Mheshimiwa Rais.

  • Kwamba usalama wa Mheshimiwa Rais hauna shaka yoyote, na uko mikononi mwa watu makini, salama, watu wazalendo wanaojali usalama wa Mheshimiwa Rais na nchi yetu, na watu wa kuaminika kabisa.

  • Kwamba tunawaomba waandishi wa habari kutojiingiza katika ubashiri usiokuwa na msingi wala tija katika suala hili, badala yake wasubiri ripoti kamili ya mamlaka husika zinazochunguza tukio hili.

  • Aidha, tunawaomba wananchi wawe na subira kuhusu tukio hilo, na kuwa watajulishwa matokeo kamili ya nini kilisababisha hali ile pale Moshi.

Nawashukuruni sana kwa kunisikiliza.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

10 Juni, 2010

 

   
 

Custom Search

Go up

 

Quick Links

Watch Television
News Archive

© www.zenjydar.co.uk - Since 2007 | Web master | Site map | www.zenjydar.co.uk - Since 2007 ©