Inaelezwa na Baraka Mfunguo
Wakati
nikiwa Tunduru nilipata simulizi
mbalimbali kuhusiana na wilaya hiyo
jinsi ilivyo tajiri wa ardhi yenye
rutuba ya kutosha pamoja na maji mengi
ya kutosha kulinganisha na wilaya
nyingine zilizopo mikoa ya Kusini.
Lakini
kilichonisisimua zaidi ni simulizi juu
ya hili bwawa ambalo hata kuletwa na
kufika hapa na mwenyeji wetu ilikuwa
shughuli kidogo na ilitulazimu tuwaombe
wenyewe ili tufike na kurudi salama.
Unaweza kulidharau kwa macho ukilitazama
lakini amini usiamini ninachokueleza
ndicho nilichoshuhdiwa na wenyeji. Bwawa
hili lina nguvu za ajabu ambapo kama
utakuwa umekwenda kwa shughuli zako na
kuhatarisha matumizi yake ikiwa ni
kukojoa, kutukana matusi na mambo
mengine ambayo ni chukizo, hakika
unapoteza maisha. Na inasemekana kila
baada ya kipindi fulani mtu hupoteza
maisha kwa kufia humo bwawani.
Bwawa hili
lililopo Kiuma wilaya ya Tunduru
linasemekana linatoa maji safi ya kunywa
pamoja na matumizi mengine ikiwamo
ufyatuaji wa tofali za udongo kwa
wenyeji. Mwaka jana wanafunzi wa shule
ya Sekondari ya Kiuma iliyopo karibu na
bwawa hilo walikwenda kuoga pamoja na
kufua nguo lakini mmoja wao hakurudi
salama.
Ilikuwaje?
Inaelezwa kwamba mara baada ya kijana
huyo kumaliza shughuli zake alikaa
pembeni ya bwawa akiwasubiri wenzake.
Lakini kadiri jua lilivyozidi kuongezeka
alihisi joto na kuonelea ni busara
akaingia bwawani ili apooze joto la
mwili wake. Wakati akiwa bwawani
kijana huyo alitamka
lugha ya matusi na maneno mabaya kuhusu
maji ya bwawa hilo ghafla akahisi nguvu
kali ikimvuta kuelekea chini. Akaomba
msaada kwa wenzake ambao walijaribu
kutaka kumwokoa wakaona nawao wanazidiwa
nguvu kwa kuvutwa ikashidnikana na
mwenzao akatokomea majini.
Baada ya mwenzao
kutokomea majini, vijana wale walikwenda
kutoa taarifa shuleni kwao kwamba
mwenzao amepotea katika maji bwawani na
wamejaribu kumwokoa wakashindwa. Wakuu
na wahusika wengine wakaanza taratibu za
uokoaji ili kusalimisha maisha ya kijana
huyo ikiwa na Mkuu wa kituo cha Kiuma
kuagiza ndege binafsi yenye wataalam wa
uokoaji kutoka Dar es salaam kuja mara
moja kumwopoa kijana huyo jitihada
ambazo zilishindikana pamoja na waokoaji
wengine. Ndipo ikalazimu kwenda kwa
wazee wa jadi ambao walifanya tambiko na
kuomba kwa muda wa siku 3 na mara baada
ya hapo kazi ya kumwopoa ikaanza.
Inaelezwa kwamba kijana huyo alipatikana
lakini nguvu ya ziada ilitumika kwani
mbali na kupatikana kwake lakini bado
walinyang'anyana wakiwa majini.
Alipoopolewa kijana huyo alikuwa tayari
amekwishafariki cha ajabu kilichoonekana
ni kutokwa na damu puani kwa kijana huyo
hali alikuwa majini kwa siku 3. Tukio
hilo lilileta simanzi kubwa katika jamii
nzima ya Kiuma na uongozi wa Kiuma
ulichukua hatua ya kuwapiga marufuku
wanafunzi wake kufika katika eneo hilo.
Walioingia kumwokoa
kijana huyo walieleza kwamba walikutana
na vitu ambavyo ni adimu kuonekana
katika hali ya kawaida katika maisha ya
binadamu. Ikiwa na sehemu ambazo hakuna
maji kabisa na kuwa kukavu kama nchi
kavu huku upande mwingine maji yakiwa
yamezunguka pamoja na matukio mengine ya
ajabu ambayo ni ngumu kumuelezea mtu
akaamini.
Inaelezwa kwamba kuna
bwana mmoja mvuvi alikwenda kutafuta
kitoweo bwawani hapo alipotwika ndoano
na kuvuta akavuta lundo la samaki wakavu
waliochomekwa katika umambo mmoja jamaa
akatimua mbio na ikawa mwanzo na mwisho
wa kukanyaga hapo. Matukio mengine ni
kama kukuta nguo zimeanikwa na wahusika
hawaonekani ama kusikia sauti za watu
zikiongea na usiwaone.

Hayo ndiyo maajabu ya
Tunduru. Tembea Uone usingoje kuambiwa.
Asiyeamini afuatilie na kujua kuhusiana
na matukio niliyoyaeleza hapo kuhusu
bwawa hilo la KIUMA.