Naibu Kamishna wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo,
mwezi uliopita mbele ya
waandishi wa habari Jijini Dar
es Salaam alieleza magari hayo
yalikamatwa katika operesheni
maalumu iliyopewa jina la
MODJADJI, kutokana na kuwapo kwa
taarifa za kiintelijensia
zilizokusanywa sehemu mbalimbali.
Taarifa za operesheni hiyo
ilifahamisha kuwa magari 10 kati
hayo yaliyokamatwa katika
operesheni ya saa 24
iliyofanyika Agosti 27 na 28,
mwaka huu ambapo yalikutwa na
kasoro mbalimbali ikiwemo
nyaraka za magari ambazo
zinatofautiana kwenye chassis.
Magari mengi yaliyokamatwa
yalionekana kuibiwa na idadi
yake kwenye mabano ni Afrika
Kusini (12), Japan (22),
Malaysia (8), Uingereza (3)
pamoja na Kenya, Australia,
Ujerumani , Slovenia , Msumbiji
na Tanzania.
Baadhi ya maeneo yaliyoongoza
kwa kukamatwa na magari hayo ya
wizi kuwa ni Mkoa wa Kinondoni
uliongoza kwa kukamatwa gari za
wizi (12) ukifuatiwa na Zanzibar
(8), Ilala (5) na Mbeya (3).
Tangu kukamatwa kwa gari hizo
hadi sasa yaliokamatwa Zanzibar
yakiwemo aina Toyota, Nissan
bado yapo katika kituo cha
Polisi cha Mkoa wa Mjini
Magharibi Mwembe Madema
yakisubiri khatima yake.
Magari hayo ya Zanzibar,
yalikamatwa katika yadi ya
Kiembesamaki inayomilikiwa na
mfanyabiashara Salim ambapo
Polisi hao waliweza kuyatambua
baada ya kuyafanyia uchunguzi
kutokana na kuwemo katika orodha
ya gari zilizoibiwa duniani.
Akizungumza na Zanzibar Leo,
Kamishna wa Jeshi la Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa,
alithibitisha kukamatwa kwa gari
hizo na bado zipo Zanzibar
taratibu zaidi zinaendelea.
Alisema uchunguzi wa suala hilo
hivi sasa umeshakamilika na
taarifa zake zinapelekwa Makao
Makuu ya Polisi Dar es Salaam,
kwa ajili ya kufanyiwa kazi
kwani taarifa za kimataifa za
upatikanaji wa gari hizo haukuwa
Zanzibar pekee.
Kamishna huyo, alifahamisha kuwa
wamechukua muda kutokana na
magari hayo yalipitia katika
njia ndefu baada ya kuibiwa
kutokana na wafanyabiashara wa
Zanzibar waliokutwa nayo wapo
walionunua kutoka Japan kupitia
Dubai na kuingizwa Zanzibar.
Hapo awali alisema kabla ya
kukamatwa magari hayo walifanya
msako wa kuyatafuta barabarani,
lakini baada ya kutofanikiwa
ndipo walipoamua kuingia katika
maduka ya magari ya baadhi ya
wafanyabishara wa Zanzibar na
kunasa idadi hiyo.
Kamishna huyo alisema kulikuwa
na mzunguuko katika kuyapata
magari hayo kwani palilazimika
pawepo ushirikiano wa
wafanyabishara walioingiza gari
hizo na kutafuta vielelezo vya
kuingizwa nchini.
Alisema baada ya kukamilisha
hatua hizo hivi sasa wanasubiri
kupata matokeo juu ya suala hilo
ambalo linasimamiwa na
'Interpol'.
Tanzania imefanikiwa kunaswa kwa
magari hayo baada ya hivi sasa
kuwapo kwa ushirikiano wa Askari
wa Kimataifa ambapo katika msako
huo pia waliweza kuwakamata
wahamiaji haramu 42, silaha
haramu 13 pamoja na risasi 506.
Wahamiaji haramu waliokamatwa ni
Wasomali 14, Warundi (24),
Wakenya (2), Mzambia mmoja na
Mkongo mmoja pamoja aina ya dawa
za kulevya zilizokamatwa katika
operesheni hiyo kuwa ni Heroin
gramu 243, bangi kilo 43.