Watumiaji
huduma za simu za mikononi wapatao
milioni nne watafikishwa mahakamani
ambako wanaweza kuhukumiwa kifungo au
faini kutokana na kushindwa kusajili
laini zao kabla ya Oktoba 15.
Mkurugenzi
msaidizi wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), Richard Kayombo
aliliambia gazeti hili jana kuwa mbali
na adhabu hiyo, simu hizo zitafungiwa.
“Sheria
mpya ya mawasiliano imeanza kutumika
kuanzia Mei 15 mwaka huu na mtu yoyote
ambaye hajasajili laini yake, atakumbana
na adhabu zilizoainishwa katika sheria
hiyo," alisema Kayombo.
“Kesho (leo)
tutakutana na kampuni zote za simu
katika kikao ambacho kitajadili agenda
mbalimbali, ikiwemo hii ya simu hizo na
adhabu wanazopaswa kupewa wahusika."
Hata hivyo,
Kayombo hakubainisha njia watakazotumia
kuwanasa wasiosajili simu na kuwapeleka
mahakamani. Kwa mujibu wa Kayombo
usajili wa simu ulioanza mwezi Juni
mwaka jana, ulimalizika Oktoba 15 mwaka
huu na yeyote ambaye alikuwa hajasajili
simu yake, atakuwa ametenda kosa
kisheria. Kayombo alieleza kuwa hadi
Oktoba 15 mwaka huu, laini milioni 16 za
simu, ambazo ni asilimia 76 ya watumiaji
milioni 20 wa simu zote, zilisajiliwa.
Kayombo
alisema kadi zote zinazouzwa kwa sasa
zinatakiwa zisajiliwe kwanza na kuzitaka
kampuni za simu za mkononi kuwapiga
marufuku mawakala wake wanaouza kadi
hizo bila kuzisajili.
Pia
alizitaka makampuni yote za simu kuwa
makini na mawakala wao ambao wanaouza
laini bila ya kusajili, akiyataka
yaamuru waache mara moja kwa kuwa
wakibainika, sheria itafuata mkondo
wake.
Katika
hatua nyingine, Kayombo alitoa wito kwa
watumiaji wote wa simu za mkononi,
kutumia vizuri simu zao bila kuwabugudhi
watu wengine.
“Sheria
zipo wazi kwa hiyo mtu atakayebainika
kutumia simu yake vibaya kwa kutukana
watu au mambo mengine kama hayo,
atachukuliwa hatua,” alieleza.